Ligi ya mabingwa barani Ulaya itaendelea tena
leo kwa michezo miwili ya mkondo wapili hatua ya robo fainali, kuchezwa
katika miji ya Leicester (England) na Madrid (Hispania).
Mabingwa watetezi wa ligi kuu nchini England,
Leicester City watakuwa nyumbani King Power wakipambana kuweka rekodi ya
kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza, pale watakapo
wakaribisha Atletico Madrid kutoka Hispania.
Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa
Jumatano iliyopita huko Vincente Cardelon, Leicester City walikubali
kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Atletico Madrid. Ili waweze kufuzu nusu
fainali Leceister City wanahitaji kupata ushindi wa mabao 2-0 na
kuendelea huku wapinzani wao Atletico Madrid wakihitaji kupata sare ya
aina yoyote ile.
Mchezo mwingine, Real Madrid wakiwa bila ya staa
wao, Gareth Bale anayesumbuliwa na majeraha ya mguu watakuwa nyumbani
Santiago Bernabeu kuwaalika mabingwa wa Ujerumani, FC Bayern Munich
ambao wametiwa chachu kwa urejeo wa mshambuliaji wao mahiri Robert
Lewandowski aliyekosa mchezo wa mkondo wa kwanza kutokana na kuwa
majeruhi.
Real Madrid wanaingia katika mchezo wa leo
wakihitaji sare ama ushindi wowote, ili waweze kufuzu nusu fainali kwa
msimu wa saba mfululizo.
FC Bayern Munich wao wataingia katika mchezo wa leo wakihitaji ushindi wa kuanzia mabao 2-0 na kuendelea.
Mara ya mwisho FC Bayern Munich kuifunga Real
Madrid ilikuwa ni mwaka 2001, pale ilipoichapa kwa bao 1-0 lililofungwa
na Mbrazil, Giovane Elber.
No comments:
Post a Comment