“@officialshetta ndugu yangu, najua unanionea gere mwenzako toka juzi Insta yote imehamia Madale… na wewe unataka kuingia kwenye huu upepo wa #Muzikisiasa…
we usijiulize ingia tu, maana mjini sasa hivi vingoma vya mapenzi
vigumu, ikiwezekana jifanye unataka kumtolea mahari Mange umuoe…kesho
mji wote wako ila kuna mawili, sentro au matusi.”
Hayo ni maneno ya utani aliyotoa wiki hii staa wa Bongo Fleva, Naseeb
Abdul ‘Diamond Platnumz’ akimtania msanii mwenzake Nurdin Bilal ‘Shetta’
ikiwa ni siku moja tu tangu aachie ngoma yake ‘Acha Nikae Kimya’, wimbo
uliozua gumzo nchini.
Kwa utani huo unaweza kuona ni namna gani matukio (kiki)
yanavyooanishwa na kazi za sanaa ambapo mastaa kadha wa kadha wamekuwa
na utamaduni wa kutengeneza matukio bandia kabla hawajatoa kazi mpya ili
kuwasogeza karibu mashabiki.
Ni mtindo unaotumiwa na mastaa wengi ulimwenguni kote, siyo jambo geni kabisa. Ingawa si wasanii wote hutumia kiki kuongeza usikivu kwa mashabiki, kwa
upande wa wasanii wa Bongo Fleva kuna sampo hiyo ya wasanii
wasioendeshwa kwa kutumia kiki.
Hapa chini nakupa listi ya wasanii wa kike wa Bongo Fleva ambao kiki
kwao siyo dili, wanapiga kazi tu. Mastaa hawa hawatoi nafasi ya kiki
kuendesha muziki wao.
Omary Ramsey anawapa heshima warembo hao na hapa tunakusogezea baadhi tu ya
mastaa wapya wa kike ambao hawatumii kiki kwenye kazi zao za sanaa bali
kazi zao nzuri ndiyo zinazowakiki mbele ya jamii.
MAUA SAMA
Huyu ni mwimbaji hodari ya nyimbo za mapenzi, ana sauti nyororo
anayoitumia vyema kuumudu ushindani uliopo kwenye Bongo Fleva. Anamiliki
hit song kali kama ‘So Crazy’, ‘Let Them Know’, ‘Sisikii’, ‘This Love’,
‘Mahaba Niue’ na ‘Main Chick’.
Zaidi ya muziki wake kumpa kiki kwenye ulimwengu wa Bongo Fleva mpaka
kuchukua tuzo ya Wimbo Bora wa Reggae (Let Them Know), hajawahi
kufikiria kutengeneza tukio ili kubusti kazi zake.
NANDY
Mrembo huyu ni balozi wa taasisi iliyoanzishwa na Naibu Spika wa Bunge,
Dk. Tulia Ackson. Heshima ambayo imekuja baada ya kuonekana msafi
ambaye hana makandokando kwenye maisha ya ustaa.
Ubalozi ni dili ambalo wasanii wengi wa kike wamelikosa kutokana na
skendo au kiki ambazo mwisho wa siku zimeondoa heshima yao. Nandy
amekuwa staa kutokana na mashabiki kumpa usikivu kupitia nyimbo zake
kama ‘Nagusagusa’ na ‘One Day’.
ROSA REE
Kutoka The Industry, lebo inayomilikiwa na Kundi la Navy Kenzo
tunakutana na rapa mwenye sauti na michano yenye mamlaka, Rosa Ree
ambaye hivi karibuni aliungana na Rick Ross katika dili la ubalozi wa
kinywaji cha Luc Beraile.
Kiki siyo sehemu ya maisha yake sababu uwezo wake wa kuchana pekee ni
kiki tosha kwenye muziki wa Hip Hop kiasi kwamba rapa mkubwa kama Joh
Makini amemtabiria makubwa huko mbeleni.
MIMI MARS
Anaitwa Marianne Mdee ambaye ni mdogo wa damu wa Vanessa Mdee. Ni
mtangazaji ambaye amejiongeza kwa kutumia talanta yake ya pili ya
uimbaji na sasa anasumbua na ngoma inayoitwa Shuga.
Hapendi sana kutumia mgongo wa dada yake ili kufika kwenye kilele cha
mafanikio. Anatambua kiki siyo afya kwa uhai wa muziki wake ndiyo maana
amekaza kwa kufanya kazi nzuri zilizompa mashabiki wa kutosha.
CHEMICAL
Ni nadra msichana mdogo kujiamini kiasi kile, rapa Chemical ni alama ya
warembo wote wenye ujasiri wa kukabili hali zote zilizopo kwenye muziki
wa Bongo Fleva.
Ni muwazi na mkweli, asiyependa kupindisha mambo. Hajawahi kutumia kiki
ili kusukuma ngoma zake. Skendo pia huwa anazikwepa kwa sababu hataki
kuzichanganya na muziki alioujenga kwa miaka mitatu sasa.
Mfano ni kipindi kile msanii Stereo alipotangaza hadharani kumpenda,
Chemical aliutatua msala ule bila kuacha madhara kwenye muziki wake.
Chukueni tano wote!
No comments:
Post a Comment