Timu ya soka ya Borussia Dortmund jana usiku ilipata pigo baada ya
kushambuliwa na milipuko mitatu muda mfupi kabla ya mchezo wake wa robo
fainali ya Kombe la Mabingwa barani Ulaya dhidi ya Monaco ya Ufaransa.
Jeshi la polisi la Dortmund kupitia mkutano na waandishi wa habari
ulioongozwa na mkuu wa jeshi hilo wa Dortmund lilieleza kuwa milipuko
yote mitatu ilikuwa imeilenga timu hiyo.
Hata hivyo, milipuko hiyo haikulipata moja kwa moja basi lililokuwa
limebeba wachezaji lakini kishindo cha mlipuko kilipelekea vioo vya gari
hilo kuporomoka na matairi kupasuka, huku mchezaji Marc Bartra
akiripotiwa kupata majeraha katika eneo la kiuno na mkononi.
Marejaha ya Bartra yametokana na vioo vilivyoruka na kumshambulia katika maeneo ya mwili wake na kupelekea kufanyiwa upasuaji. Mwendesha mashtaka wa serikali ameeleza kuwa kuna barua ambayo
ilikutwa karibu na eneo la tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea
dhidi yake.
Akieleza kwa ufupi, amesema barua hiyo ilikuwa inaeleza kuhusu
uhusika wa shambulizi dhidi ya timu hiyo, ikiaminika kuwa imetoka kwa
wapangaji wa tukio hilo.
Kadhalika, polisi wamedai kuwa wamepata vitu vinavyoweza kuunganishwa
kwenye tukio hilo vikiwa katika hoteli ambayo timu hiyo ilifikia.
Kutokana na tukio hilo baya, mchezo kati ya Dortmund na Monaco uliahirishwa hadi Jumatano. Wakati tukio hilo likitokea, tayari mashabiki zaidi ya 80,000
walikuwa ndani ya uwanja wakisubiri mtanange huo, ambapo Jeshi la polisi
liliwaomba kutoondoka hadi hali itakapokuwa shwari. Baada ya muda wote
waliondolewa wakiwa salama.
Raia wa Dortmund walieleza kufurahishwa na ushirikiano uliooneshwa na
mashabiki wa Monaco, hali iliyopelekea kuwakarimu wakiwaalika kupitia
mitandao ya kijamii kuwa wangewapa malazi kwa usiku huo.
No comments:
Post a Comment