Klabu ya Arsenal, huenda ikakubali kumuachia mshambuliaji wake kutoka
nchini Chile Alexis Sanchez mwishoni mwa msimu huu, kufuatia
sintofahamu inayoendelea kuchukua nafasi katika suala la kutosaini
mkataba mpya.
Arsenal wapo tayari kumuuza Sanchez kwa mabingwa wa soka nchini
Ufaransa Paris Saint-Germain, ambao wameonyesha nia ya dhati ya
kumsajili. Dhumuni la The Gunners kufikiria biashara hiyo, limetokana na hitaji
la kutaka kumpeleka mbali na mji wa London mshambuliaji huyo, ambaye
ananyatiwa na The Blues (Chelsea).
Taarifa za awali zinaeleza kuwa PSG wapo tayari kutuma ofa ya Pauni
milioni 50 huko kaskazini mwa jijini London, ili kufanikisha usajili wa
Sanchez wakati wa usajili wa majira ya kiangazi.
Hata hivyo bado meneja wa Arsenal Arsene Wenger, ana matarajio
makubwa ya kuendelea kuzungumza na mshambuliaji huyo mwenye umri wa
miaka 28, ili akubali kusaini mkataba mpya.
Kuhusu suala la ahadi ya kumlipa mshahara wa Pauni laki tatu
(300,000) kwa juma, Wenger amekanusha taarifa hizo ambazo zilisambaa
katika mitandao ya kijamii mwishoni mwa juma lililopita.
Wenger aliwaambia waandishi wa habari, hajawahi kumwambia ama
kumuahidi mshambuliaji huyo mshahara wa Pauni 300,000 kwa juma, zaidi ya
uzushi huo kupita katika mitandao ya kijamii.
Sanchez tayari ameshaifungia Arsenal mabao 22 msimu huu, na amekua
msaada mkubwa katika kikosi cha The Gunners, tangu aliposajiliwa
Emirates Stadium mwaka 2014, akitokea FC Barcelona.
No comments:
Post a Comment