Tuesday, 28 March 2017

Simba SC yajilipua kwa Hajib, Mkude



Klabu ya Simba ipo tayari kumpa mkataba mpya, Nahodha wake, Jonas Mkude utakaomruhusu kuondoka akipata timu nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe jana ofisini kwake, Mbezi, Dar e Salaam.

Hans Poppe amesema wapo kwenye mazungumzo ya mkataba mpya na kiungo huyo, ambayo yanaendelea vizuri. Zacharia Hans Poppe amesema wapo kwenye mazungumzo ya mikataba mipya na Jonas Mkude na Ibrahim Hajib

“Wakala wa Mkude anaishi Afrika Kusini, na sisi hatuna shida kuwa na kipengele cha kumruhusu kwenda nje akipata timu. Kwa hivyo tunatarajia tutafikia makubaliano katika mazungumzo yanayoendelea,”amesema Poppe.

Pamoja na hayo, kumekuwa na taarifa za Mkude kutaka kwenda kucheza soka ya kulipwa Afrika Kusini ambako alikwenda kwa majaribio mwaka jana

Mkude aliyedumu Simba SC tangu mwaka 2011 baada ya kupandishwa kutoka kikosi cha vijana, anatarajiwa kumaliza mkataba wake Juni mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Hans Poppe amesema Simba haina taarifa yoyote kuhusu mshambuliaji wake, Ibrahim Hajib kutakiwa na klabu ya Haras El Hodoud ya Misri.

“Ni kweli Hajib alikwenda majaribio Misri na ikaripotiwa amefuzu, lakini tangu hapo ile klabu haijawasiliana na sisi kwa chochote, kwa hivyo hatujui kinachoendelea,”amesema Poppe.

Hajib alikuwa Misri kati ya Desemba na Januari kwa majaribio, ambako ilielezea amefuzu – lakini klabu hiyo ya Ligi Kuu ikashindwa kukamilsha uhamisho wa mchezaji huyo kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa Januari mwaka huu.

Sasa inatarajiwa Hajib anaweza anaweza kuondoka Simba SC kama mchezaji huru Juni mwaka huu atakapmaliza mkataba wake.

No comments:

Post a Comment