Agosti 2, 2016 staa mwenye jina kubwa ulimwenguni Shawn Carter ‘Jay Z’ alitimiza malengo yake ya muda mrefu kwa kuwa msanii wa kwanza duniani kumiliki mtandao ambao umewawezesha waandishi wa muziki na wanamuziki mastaa wakubwa duniani kufaidika na jasho lao kwa kuuza kazi zao za audio na video kwa mashabiki wao duniani kote.
Mtandao huo unaitwa Tidal ambao ulianzishwa mwaka 2014 na Kampuni ya
Kiswedishi iitwayo Aspiro, baadaye ukamilikiwa na Project Panther Bidco
L.T.D kabla ya Jay Z
kuununua mtandao huo ambao mpaka sasa una zaidi ya nyimbo milioni
ishirini na tano (25) za audio na zaidi ya video elfu themanini na tano
(85) huku mastaa wakiwemo Drake, DJ Khaled, Fat Joe, Nick Minaj na
wengine wengi wakiweka kazi zao na kukunja mkwanja wa maana.
Huyo ndiye Jay Z, aliyemhamasisha mwanamuziki mwenye mafanikio makubwa
Bongo, Diamond Platnumz kuwa msanii wa kwanza Tanzania kumiliki mtandao
wake unaoitwa www. wasafi. com ambao unawawezesha wanamuziki kuweka kazi
zao za audio na video huku wakiziuza kwa shilingi 300, ambapo mpaka
sasa baadhi ya mastaa waliojitokeza na kuweka kazi zao ni pamoja na
Profesa J, Navy Kenzo, Bill Nas, Ray C, Barnaba, Belle 9, Chegge na
Temba.
Tofauti ya Jay Z na Diamond ni kwamba, Mmarekani huyo alipoununua
Mtandao wa Tidal, malengo yake makubwa ni kuuza muziki na kuwasapoti
wasanii wenzake kisha kila mmoja kupiga mkwanja, kwa wanaokumbuka hata
kauli mbiu ya kuutangaza mtandao huo ilikuwa ni Tidal For All kwa
tafsiri isiyo rasmi ni kwamba Tidal ni kwa ajili ya watu wote. Ukirudi
kwa Diamond kinachoonekana nyuma ya mtandao wake wa www. wasafi.com ni
mtego kwa mastaa Bongo, yaani anawasaidia kuuza kazi zao lakini wao
wanatangaza lebo yake, wasanii wake na biashara zake zote zenye nembo ya
wasafi.
Hili halionekani kwa Jay Z ambaye ana lebo yake ya Roc- A- Fella Records
na Kampuni ya Roc Nation. Maana angeweza kuubadilisha Mtandao wa Tidal
na kuita jina mojawapo la hayo ya kampuni zake kisha kujitangaza zaidi
duniani kupitia wasanii ambao wameweka kazi zao kwenye mtandao huo.
Lakini kwa upande wa Diamond, mtego huo unaweza kuuona pale ambapo
wasanii walioweka nyimbo zao kwenye mtandao huo wanapokuwa wanatangaza
zinapatikana wapi! Lazima waseme katika Mtandao wa www.wasafi.com ambao
unamilikiwa na Diamond Platnumz ambapo huko pia matangazo ya biashara
zake ameweka.
Kwa hiyo kutokana na ukweli huu, baada ya miaka mitano mbele kama
Diamond akifanikiwa kuutangaza mtandao huu vizuri na wasanii wengi
kuweka nyimbo zao, asilimia 85 ya wanamuziki Bongo watakuwa wanamtangaza
yeye, vijana wake na biashara zake. Ndiyo mahesabu ya kibiashara
yanayoonekana katika mtandao wake.
Ni ukweli aweke kazi zake kwenye mtandao wake, inaweza kuwa ni kweli
lakini katika sura nyingine, anatafuta urafiki wa kibiashara. Ili Kiba
aingie mkenge na baadaye kuwa wakala wake wa kumtangaza, wasanii wake
pamoja na biashara zake zingine kwa maana mashabiki wakimfuata Ali Kiba
www. wasafi. com wanakuwa wamemfuata Diamond Platnumz. Unaweza kukumbuka
pia Diamond alivyoua ushindani baina yake na Rich Mavoko pale tu
alipomfanya kuwa msanii wake.
Hata hivyo, ninampongeza Diamond kwa maono yake, anaitendea haki ile
kauli inayosema mwenye nacho ataongezewa, kikubwa tu asirudi nyuma na
asonge mbele maana kwenye mambo ya mtandao historia inaonyesha mkali
huyu ni mzuri kwa kuanzisha lakini baadaye hupotelea kusikojulikana.
Kwa kumbukumbu, aliwahi kuanzisha mtandao uitwao this is Diamond,
akaupotezea akaanzisha mwingine Forever Diamond, akaupotezea na mtandao
mwingine ni ule ambao mwisho kuposti ni Agost mwaka jana alipokuwa
kwenye ‘tour’ ya Wimbo wa Salome uitwao Diamond Platnumz ambao nao
anaonekana kupotezewa.
No comments:
Post a Comment