Inawezekana mpaka leo hii bado Bongo Muvi wanajifikiria namna ya kutoka na
kutengeneza pesa ya nguvu, wanaoandaa filamu hawajui ni kwa namna gani
wanaweza kutoka na kuweka ladha tofauti katika filamu zao.
Wakati sisi tunajifikiria hivyo, wenzetu hasa Hollywood wamepiga
hatua na sasa hivi kuna vita kali inaendelea katika watengenezaji wa
filamu nchini Marekani, ni vita kubwa ambayo inawafanya kutengeneza pesa
kila siku iendayo kwa Mungu.
Kila mwaka kampuni za muvi, Warner Bros, Marvel na 20th Century Fox
zinakuja na mawazo mapya, ni kwa namna gani wanaweza kutengeneza fedha
kwa kuwaandaa waigizaji wa ajabu (comic) ambao sasa hivi wamekuwa
wakipendwa na kuwafanya watu kuingiza fedha kwa kiasi kikubwa.
MAMBO YAPO HIVI
Walianza Warner Bros. Hii ni kampuni inayomilikiwa na wanaume wanne
waliotoka kwenye familia ya Warner. Baada ya kuingia kwenye filamu
wakawaandaa wahusika wao kama Superman, Batman, Joker, Green Lantern na
wengineo miaka ya 1970.
Waliikamata dunia, walitengeneza sana fedha kiasi kwamba leo
unaposema Superman au Batman kila mtu anawafahamu. Baada ya miaka mingi
na kuona kwamba Marvel wanakuja kasi, wakaongeza wahusika wengine kama
Wonder Woman na wale wote wanaopatikana kwenye filamu ya Suicide Squad
ikiwa na Will Smith.
Wakati Warner Bros wakiendelea, kwa upande wa Marvel, walichokifanya
ni kuwaweka wahusika wao. Wakamtengeneza Spiderman, kweli akawa maarufu,
akapendwa na kuwapa fedha nyingi, baada ya hapo wakawatengeneza
Ironman, Hulk, Captain America, Black Panther na mwaka huu
wamemtengeneza mwingine aitwaye Dr. Strange.
WAWAKUSANYA PAMOJA
Wakati utata wa wahusika wa kampuni ipi wapo bomba zaidi ya wengine,
walichokifanya Marvel ni kuwachukua wahusika wake wengi na kuwaweka
pamoja kwa kutengeneza muvi iitwayo Avengers ambayo ilikuwa na wahusika
kama Ironman, Hulk, Thor, Black Widow baadaye wakamuweka BlackPanther,
Antman, Spiderman ambao waliingia kwenye muvi ya Captain America: Civil
War.
Kwa ujumla Avengers imeingiza dola bilioni 1.405 (zaidi ya shilingi
trilioni mbili). Mbali na hayo, pia wakaanzisha filamu za Deadpool, X
Men ambayo zimekusanya mastaa wengi wakiwemo Magneto, Professor X na
wengine wengi na kwa filamu hizo pia wakafanikiwa kuingiza kiasi kikubwa
cha fedha.
Warner Bros wakaona kama wamefunikwa, na wao walichokifanya ni
kutengeneza muvi ambayo ilikuwa na waigizaji wao kwa pamoja,
wakatengeneza ya Superman vs Batman iliyotoka mwaka huu, humo wakamuweka
Wonder Woman na filamu hii ikaingiza dola bilioni 872 (zaidi ya
trilioni moja) na inaendelea kuingizampaka leo.
20th CENTURY FOX WAZEE WA KIMYAKIMYA
Wakati hayo yote yakiendelea, 20th Century Fox hawana hofu,wamekaa
pembeni na wanaangalia jinsi mchezo unavyochezwa na wenzao. Wanajiamini
kwa sababu wana mtu anaitwa James Cameron ambaye ndiye aliyetengeneza
muvi za Terminator zilizochezwa na Schwarzenegger, Titanic na Avatar.
KWA NINI 20th CENTURY WANAMUAMINI CAMERON?
Huyu jamaa anaweza kuitwa ‘genius’ kutokana na filamu zake
zinavyobamba. Kwanza unatakiwa kujua kuwa filamu yake ya Titanic ndiyo
iliyokuwa ikiongoza kwa kuingiza fedhanyingi duniani kuliko filamu zote
kabla ya rekodi hiyo kuvunjwa na Avatar mwaka 2009.
Mpaka sasa filamu hiyo (Titanic) imeingiza dola bilioni 2.187 (zaidi
ya trilioni 4.5). Baada ya hapo, kuonyesha k w a m b a alikuwa si mtu wa
mchezomchezo, akaandaa filamu nyingine iitwayo Avatar ambayo ilivunja
rekodi na kuipitia Titanic, mpaka sasa ndiyo imekuwa filamu iliyoingiza
kiasi kikubwa cha fedha, dola bilioni 2.788 (zaidi ya trilioni 6).
Hawa washikaji wanawaangalia wenzao (Marvel na Warner Bros)
wanavyopambana kila mwaka kwa kutengeneza filamu zao kwa kuwaweka mastaa
wengi mno ila tangu 20th Century Fox watengeneze filamu yenye watu wa
ajabu ya Avatar mwaka 2009, mwaka huu wanakuja na Avatar 2 ambayo
vipande vyake (trailer) vitaanza kuonyeshwa mwaka huu.
Wanachojua ni kwamba filamu yao itakuja kuzikimbiza zote za Avengers
na Superman vs Batman kwa kuwa tu wana mtu sahihi. Je, unahisi Avatar 2
itaifunika ile ya kwanza na kuuza zaidi? Unahisi hawa Marvel na Warner
Bros wataweza kuwafunika 20th Century? Yetu macho.
No comments:
Post a Comment