Sunday 5 July 2015

Hawa ndio Mastaa 10 wenye nguvu zaidi Afrika Mashariki – 2015


1. Lupita Nyong’o – Kenya

Lupita Nyong’o ni jina maarufu mno duniani kwa sasa. Umaarufu wake kwa Afrika Mashariki ulianzia kwenye tamthilia ya mwaka 2009, Shuga. Umaarufu wake duniani, ulitokana na kuigiza filamu iliyoshinda tuzo za Oscar, ’12 Years A Slave.’
Kwenye filamu hiyo aliigiza kama Patsey, mtumwa wa kike aliyejikuta akipata shida kubwa kwa kazi ngumu za mashambani. Uhusika wake kwenye filamu hiyo ulimfanya mwaka jana ashinde kipengele cha muigizaji msaidizi wa kike bora kwenye tuzo za Oscar. Ushindi huo ulimfanya kuwa muigizaji wa kwanza kutoka Afrika kuwahi kushinda tuzo hizo za thamani.
Pia aliigiza kama mhudumu wa ndege kwenye filamu ya action ya mwaka jana, Non-Stop akiwa na Liam Neeson na Julianne Moore. Mwaka huu ameigiza filamu iitwayo Queen of Katwe na Star Wars Episode VII: The Force Awakens.
Umaarufu wake ulimpa deals zaidi ikiwa ni pamoja na kuwa kisura wa kampeni ya Miu Miu akiwa na walimbwende wengine, Elizabeth Olsen, Elle Fanning na Bella Heathcote. Alionekana kwenye majarida makubwa ya fashion duniani yakiwemo Dazed & Confused huku akiwa mwanamke wa pili wa Afrika na wa nane mweusi, kukava jarida la Vogue.
April mwaka jana, jarida la People lilimtaja Lupita kama mwanamke mrembo zaidi duniani katika issue yake ya ’50 Most Beautiful.’
2015, Nyong’o alikava jarida la Lucky, Harper’s Baazar’s (UK) na MujerHoy la Hispania.
Wiki hii Lupita amerejea nchini Kenya ambako alitangazwa pia kuwa balozi wa taasisi ya WildAid inayojihusisha na kampeni dhidi ya ujangili hususan wa tembo.


2. Diamond Platnumz – Tanzania

Diamond amekuwa si jina maarufu Afrika Mashariki peke yake na sasa miongoni mwa wasanii wakubwa kabisa barani Afrika. Mwaka huu peke yake ametengeneza nyimbo kubwa na collabo na wasanii maarufu Afrika zilizoshika charts kwenye vituo vya redio na runinga vikubwa. March 27 aliachia video ya wimbo wake wa Mduara, ‘Nasema Nawe’ aliomshirikisha Khadija Kopa ambao haukuishia kufanya vyema Afrika Mashariki peke yake, bali Afrika nzima. Hadi sasa video yake imeangaliwa kwenye mtandao wa Youtube kwa zaidi ya mara milioni 2.7.
Collabo yake kubwa kwa sasa ni ‘Nana’ aliyomshirikisha Flavour ambayo licha ya kushika chart za redio na TV Afrika ikiwa ni pamoja na kuwa namba moja kwenye kituo cha Trace TV, video ya wimbo huo ni miongoni mwa zile zinazoangaliwa kwa kasi zaidi kwenye Youtube barani Afrika, ikiwa na views zaidi ya milioni 2.1 tangu iwekwe May 29. Bila kusahau mwaka jana alishirikishwa kwenye nyimbo zilizohit za wasanii wa Nigeria, likiwemo kundi la Bracket na Waje.
Hivi karibuni tu video mbili za nyimbo alizoshirikishwa na wasanii wakubwa wa Nigeria zimetoka – Nakupenda aliyoshirikishwa na Iyanya na Love Boat aliyoshirikishwa KCEE.
Pia aliingia studio kurekodi wimbo aliorekodi na msanii wa Afrika Kusini, Donald. June 13 alishinda tuzo mbili kwenye KTMA 2015. Mwaka huu ametajwa kuwania vipengele vitatu kwenye tuzo za MTV MAMA na ni miongoni mwa wasanii watakaotumbuiza July 18 kwenye utoaji wa tuzo hizo, Durban, SA. January mwaka huu staa huyo alikuwa mmoja wa wasanii waliotumbuiza kwenye tuzo za Glo CAF jijini Lagos, Nigeria.

3. Wema Sepetu – Tanzania

Umaarufu wa Wema Sepetu na kuendelea kutengeneza vichwa vya habari Afrika Mashariki, unaendelea kuwepo kutokana na uhusiano wake uliokufa na Diamond miongoni mwa mambo mengine. Wema bado ameendelea kuwa staa wa kike mwenye mashabiki na ushawishi mkubwa nchini Tanzania.
Mwaka huu alishinda tuzo ya muigizaji wa filamu wa kike anayependwa zaidi kwenye Tuzo za Watu. Alisafiri hadi nchini Ghana kwenye kutengeneza filamu na muigizaji wa maarufu wa huko, Van Vicker, ambayo inatarajiwa kutoka mwishoni mwa mwaka huu. Ameendelea kutengenezwa vichwa vya habari kutokana na kutangaza nia ya kuwania nafasi ya ubunge wa viti maalum kupitia CCM, mkoani Singida. Kama mambo yakimwendea vyema, huenda jina lake mwaka huu likabadilika na kuwa Mheshimiwa Wema Sepetu.

4. Zari the Bosslady – Uganda

Kabla ya kukutana na Diamond, Zari The Bosslady alikuwa maarufu nchini Uganda. Alijulikana kwa urembo wake na utajiri mkubwa aliokuwa nao kupitia aliyekuwa mumewe, Ivan. Alifahamika kama mwanamke anayemiliki magari ya kifahari, mijengo na biashara kubwa. Umaarufu wake umekuja kukua zaidi baada ya kukutana na Diamond Platnumz na kuanzisha uhusiano ambao sasa umewafanya kuwa couple yenye nguvu zaidi Afrika Mashariki. Kwa sasa wawili hao wanatarajia kupata mtoto wao wa kwanza. Mtoto huyo bila shaka ana nafasi kubwa ya kuwa mtoto maarufu zaidi Afrika Mashariki.

5. Vanessa Mdee – Tanzania

Vanessa anafahamika kama msanii wa kike kutoka Afrika Mashariki anayejituma zaidi kuliko wote. Mwaka huu ameshiriki kwenye kampeni nyingi za kimataifa. Alishiriki kwenye kampeni ya One Organisation ambapo aliungana na wasanii wengine wa Afrika kuimba wimbo uitwao Strong Girl. Pia aliungana na mastaa wakiwemo Lupita Nyong’o, Hasheem Thabeet, Jacqueline Ntuyabaliwe na Alikiba kama mabalozi wa WildAid na kampeni dhidi ya mauaji ya tembo.
Mwaka huu ametajwa kuwania kipengele cha msanii bora wa kike kwenye tuzo za MTV MAMA. Wimbo wake ‘Nobody But Me’ aliomshirikisha rapper wa Afrika Kusini, K.O, ni miongoni mwa nyimbo zinazofanya vizuri Afrika kwa sasa. Mwezi ujao ataonekana kwenye jarida maarufu la Marekani la Essence kwenye toleo lake la dunia (global issue). Ni balozi wa Samsung na Crown Paints.

6. Millen Magese – Tanzania

Happiness Millen Magese @ladivamillen amejipatia umaarufu mkubwa mwaka huu kutokana na kuwa balozi kwenye kampeni aliyoanzisha mwenyewe ya tatizo la Endometriosis ambalo limepelelekea afanyiwe upasuaji kwa takriban mara 13 na kumfanya awe mgumba. Millen ameanzisha kampeni ya kukuza uelewa wa ugonjwa huo na kuwataka wanawake wenye tatizo hilo kutooana aibu kujitokeza kuomba msaada lakini pia kuwataka wanaume wenye watu wao wa karibu walio na tatizo hilo kuwavumilia. Kutokana na jitihada hizo pamoja na kuwa mstari wa mbele katika kusaidia watu wasiojiweza, June mwaka huu alitunukiwa tuzo ya Global Good ya BET Awards.

7. Eddy Kenzo – Uganda

Jina la Edrisa Musuuza maarufu kama Eddy Kenzo halikuwa maarufu sana kwa Tanzania na Kenya kabla ya June mwaka huu kushinda tuzo ya BET ((Best Viewers’ Choice International Act). Anahamika zaidi kwa hit yake Sitya Loss. Wimbo huu ulifahamika duniani kupitia video ya Youtube ya vijana wa mtaani waliokuwa wakicheza wimbo huu. Video hii ilikuwa maarufu kiasi cha kuwepo na ombi (petition) ili vijana hao waweze kuhojiwa kwenye The Ellen DeGeneres Show. Hadi sasa video hiyo ina views zaidi ya milioni 11. 9.
Kenzo ameshatumbuiza kwenye majiji 15 ya Marekani. Ametembelea na kutumbuiza kwenye majiji kibao duniani. Alitumbuiza kwenye fainali za mataifa ya Afrika.

8. Sauti Sol – Kenya

Bien-Aimé Baraza, Willis Chimano, Delvin Mudigi na mpiga gitaa wao Polycarp Otieno ndio wanaunda kundi la Sauti Sol.
Mwaka huu walitajwa kuwania tuzo za BET japo hawakufanikiwa kushinda. June 13, walichukua tuzo ya wimbo bora wa Afrika Mashariki kwenye KTMA 2015 na wimbo wao uliokuwa anthem ya Afrika Mashariki, ‘Sura Yako.’ Mwaka huu wanawania kipengele cha kundi bora kwenye tuzo za MTV MAMA. Kwa sasa wapo kwenye ziara ndefu nchini Marekani.

 

9. Alikiba – Tanzania

King Kiba kama anavyojiita, aliufungua mwaka 2015 kwa kishindo na hakuna anayeweza kubisha kuwa jamaa huyu ana ushawishi mkubwa nchini Tanzania. Milango yake ya umaarufu nje ya Tanzania imefunguka tena mwaka huu baada ya kuwa kimya kwa takriban miaka mitatu.
Video ya wimbo wake ‘Chekecha Cheketua’ ilichezwa kwa mara ya kwanza kwenye kituo cha Trace Urban na kuendelea kupata rotation ya mara tano kwa siku. Mwaka huu Alikiba alishinda tuzo ya muimbaji wa kiume anayependwa kwenye Tuzo za Watu na kushinda tuzo takriban sita kwenye KTMA 2015.
Mwaka huu pia ameungana na wasanii wengine wa Afrika kwenye msimu wa tatu wa kipindi cha Coke Studio Afrika huku akitengeneza timu na msanii wa Kenya, Victoria Kimani. Pia aliungana na Lupita Nyong’o, Vanessa Mdee na K-Lynn kama balozi wa WildAid katika kampeni dhidi ya mauaji ya tembo.

10. Idris Sultan – Tanzania

Ushindi wa $300,000 wa shindano la Big Brother Africa mwaka jana, umemfanya Idris kuwa miongoni mwa mastaa wakubwa Afrika kwa sasa. Japokuwa hajaanza kufanya miradi mingi, ukubwa wa shindano hilo umeendelea kuliweka jina lake kwenye headlines. Lakini pia uhusiano wake na mshiriki mwenzie wa shindano hilo, Samantha umewafanya wawili hao kuokota headlines za hapa na pale kwenye vyombo vya habari vya Afrika. Idris anafahamika kwa vituko vyake na huenda akawa na nafasi kubwa ya kuingiza fedha nyingi kupitia kipaji hicho miongoni mwa vingi alivyo navyo.

-Bongo 5
Jiunge Nasi na Huku Pia, Kwa Kubofya

No comments:

Post a Comment