Friday, 25 September 2015

Aiyola ya Harmonizer yazidi kuwateka Wanaijeria, Ye mwenyewe afunguka haya


UKIZUNGUMZIA miongoni mwa vichwa vya Bongo Fleva vinavyokuja kwa kasi kwa sasa ni wazi utamzungumzia msanii, Rajabu Abdulkhali ‘Harmonizer’ ama wengi wanamfahamu kama ‘mdogo’ wa Diamond kutokana nakufanana kwao sura na muonekano.

 
 Harmonizer amekuja kasi kunako muziki wa Bongo Fleva ambapo ndani ya wimbo mmoja alioutoa mwanzoni mwa Agosti wa Aiyola umemfanya kuwa katika ramani ya kimataifa ya muziki huu wa Bongo Fleva.

Ngoma hiyo tangu alipoitoa amepata sapoti kubwa kutoka kwa mastaa wa Afrika kama vile KCEE, Yemi Alade, Victoria Kimani (wote Nigeria), Mafikizolo, Donalds (Afrika Kusini) pamoja na Juliet Ibrahim (Ghana) ambapo wote kwa nyakati tofauti wamekuwa wakitumia mitandao yao ya kijamii kuupaisha kwa kuachia kava na hata vipande vya wimbo huo.

Harmonizer ambaye yupo chini ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) amekuwa msanii wa kwanza kutoka ndani ya lebo hiyo inayosimamiwa na Nasibu Abdul ‘Diamon Platnumz.’

Katika makala haya, Harmonizer anafunguka zaidi;

Vikwazo vipi umepitia katika muziki?
Kikubwa nakumbuka ilikuwa mwaka 2011 niliwahi kudhulumiwa shilingi 30,000 katika studio kubwa tu hapa Bongo (jina kapuni) na ilifika kipindi nikataka kukata tamaa kabisa ya kuendelea na muziki.

Shoo gani hutaisahau katika maisha yako ya muziki?
Mwaka jana kulifanyika Tamasha la Serengeti Fiesta kwenye mwezi wa 10 pande za Mtwara. Nikapewa mchongo kuwa kule ninaweza kuonana na wasanii wakubwa.

Nikafunga safari na kufikia katika hoteli moja, lakini kesho yake nikiwa njiani naelekea kwenye shoo usiku, vibaka wakanivamia na kunikwapua pesa, simu, tisheti na viatu ikabidi nirudi hotelini niuze vitu vyangu kwa ajili ya kupata nauli ya kurudi Dar.

Ulikutana vipi na Diamond?
Nilipotoka Mtwara kwenye Fiesta na kurudi Dar, nilikutana na DJ Milazo akanipatia namba ya Diamond.

Nikakaa na namba hiyo ya simu kwa takribani miezi miwili nikijiuliza nitaanzaje kumpigia simu na kujieleza akanielewa. Siku moja nikajipa moyo wa kijasiri baada ya kuliona tangazo kwenye gazeti la shoo yake iliyofanyika Sikukuu ya Chrismas akiwa na msanii wa Taarab, Mzee Yusuf ambayo ilikuwa ikifanyika Dar Live ikijukana kama Usiku wa Wafalme. Tangazo hilo likanifanya nimtumie meseji kwa kuandika;
Oy Mondi Bin Laden! Akanijibu;
Oy!

Kwa kweli nilijisikia faraja kweli hata marafiki zangu nilikuwa nawaonesha meseji ile, nikamtumia tena meseji nyingine kuwa mimi naitwa Harmonizer nafanya muziki, nilikuwa naomba nije kutambulisha wimbo wangu katika shoo yako ya Dar Live.

Alinijibu kiustaraabu kuwa wasiliana na huyu mtu nitakuombea kwa sababu shoo siyo ya kwangu. Akanitumia namba ya kaka yake anaitwa Ricardo nikawasaliana naye na kuniita Dar Live.

Nikamuomba jamaa mmoja anishuti video na kesho yake asubuhi nikamtumia kipande cha video Diamond, akaniuliza nipo katika menejimenti yoyote nikamwambia hapana akaniuliza nyimbo nilizozifanya nikamtumia.

Akanipa jibu moja tu kuwa ameenda India kumuuguza mama yake kwa hiyo akirudi atanicheki. Akarudi na kuniita kwenye ofisi zake Sinza-Mori na kuniweka katika lebo yake na kufanikiwa kutoka na Wimbo wa Aiyola.

Mipango ya video na ngoma nyingine?
Kwa sasa hivi siwezi kusema sana kwa kuwa nipo kwenye menejimeti nawaachia wao japokuwa kuna kolabo nyingi za nje ya Afrika ambazo wamekubali kazi yangu na kutaka wanishirikishe kwenye kazi zao. Mashabiki wategemee video ya ngoma hii itakayokuwa ya kimataifa kwani tutaitengeneza nje ya nchi.

 -Globalpublishers

Jiunge Nasi na Huku Pia, Kwa Kubofya

 

No comments:

Post a Comment