Kwenye moja ya mahojiano ya gazeti la Mwananchi na msanii wa muziki wa Bongofleva, Faustina Mfinanga ‘Nandy’ aliulizwa, je, kuna bifu kati yako na lebo ya Wasafi? Nandy akajibu “hapana.”
Akaulizwa, je Wasafi ni washindani wako namba ngapi kwenye orodha ya wapinzani wako, akajibu yeye hafanyi muziki kushindana na mtu yeyote, sio Wasafi wala sio lebo yoyote chini, bali anafanya muziki kwa nafasi yake.
Hayo yalikuwa majibu mazuri kutoka kwa Nandy na huenda yamejaa ukweli tupu, lakini ubaya ni kwamba matukio yanayoendelea kati ya Nandy na Wasafi yanakinzana na majibu.
Matukio yanaonyesha pande mbili hizo zina ushindani na hata kama haupo hawana budi kuukubali kwa sababu unatoka mtaani kwa mashabiki. Na kwa sababu hiyo, leo tunaangalia jinsi kolabo zinazomfanya Nandy na Wasafi kuwa kama Simba na Yanga, jinsi zinavyothibitisha kuwa kweli wawili wana lao.
Kolabo na Harmonize
Miezi sita tangu msanii Harmonize atangaze kujivua ngozi ya WCB alinaswa na Nandy na wakafanya kolabo na ikawa ni wimbo gumzo mtaani. Wimbo unaitwa Acha Lizame na mpaka sasa umekusanya watazamaji zaidi ya milioni 7 kwenye Youtube.
Wimbo huo ulikuwa ni moja ya matukio yalichatiza kuwa huenda ni kweli Nandy na Wasafi wanapigana vikumbo kwa sababu kwa kipindi chote cha maisha ya muziki wa Nandy hakuwahi kusikia kolabo yake na msanii kutoka Wasafi licha ya kwamba wengi anaendena nao kimuziki.
Labda hawapo kwenye mipango yake, lakini mbona mara tu baada ya Harmonize kujitoa WCB alimdaka na kufanya naye kazi? Hiyo ilitafsirika kuwa kumbe Nandy alikuwa anatamani kufanya kazi na mastaa wa Wasafi au mastaa wa Wasafi wanamtamani Nandy lakini matamanio nayo yanashindwa kuwa kweli kwa sababu pande mbili hizo zina mvutano.
Kolabo na Joeboy
Tangu Wasafi wamtambulishe malkia wao Zuhura Kopa ‘Zuchu’, Nandy amekuwa akishindanishwa sana na mkali huyo wa wimbo wa Sukari. Ni ushindani ambao haukwepeki kwa sababu wanafanya muziki wa aina moja Bongofleva, jinsia moja wanawake, umri sawa miaka 27 kwa 28 pia wote wanaimba vizuri.
Sasa miezi miwili iliyopita Zuchu alitoa wimbo wa mwisho kwa mwaka 2020 ukaitwa Nobody akimshirikisha msanii kutoka Nigeria, Joeboy. Halafu wiki nane zilizofuata Nandy naye akaachia wimbo ukaitwa Number One akiwa amemshirikisha Joeboy.
Hiyo ilitengeneza taswira ya kwamba huenda ni kweli wawili hawa wana upinzani ambao hawataki kuusema kwa maneno, bali matendo.
Huyu akifanya hili huyu anafanya lile kama Simba na Yanga. Matokeo yake ni kwamba imechochea zaidi kushindanishwa. Na sasa watu sio tu wamepata fursa ya kushindanisha Nandy na Zuchu, bali wanashindasha wimbo wa Nandy na Joeboy na Zuchu na Joeboy.
Kolabo na Koffi
Kubwa kuliko ni kwamba hivi majuzi Nandy alikuwa pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kumpokea Koffi Olomide kwa ajili ya kuja kufanya naye video ya wimbo wao ambao tayari wameutengeneza na kuupa jina la Leo.
Mbaya zaidi ni kwamba tukio hilo limetokea wiki nne tangu msanii wa Wasafi, Diamond Platnumz naye ampokee Koffi nchini kwa ajili ya kurekodi naye wimbo unaoitwa Waah ambayo tayari umetoka na kuvunja rekodi kibao.
Hii inaendelea kutengeneza sababu za mashabiki kuamini kwamba huenda ni kweli pande hizi mbili yaani Nandy na timu nzima ya WCB wana ushindani.
Kolabo na Alikiba
Iko wazi kwamba mpinzani namba moja wa Dimaond na WCB nzima ni Alikiba, labda sio jambo rasmi lakini angalau ndivyo inavyofahamika na watu wengi. Na mara kadhaa imeonekana kuwa wasanii wanaoweza kufanya kolabo na Alikiba ni wale ambao wanaonekana hawana ukaribu na WCB. Mfano wa wasanii hao ni Aslay, Darassa na sasa Nandy anaingia kwenye orodha hiyo kwa sababu miezi miwili iliyopita aliachia wimbo wa Nibakishie alioshirkiana na Alikiba.
Kuhusu ushindani
Ukitazama biashara zote zilizofanikiwa duniani zilifanikishwa na mambo mawili makuu. Kwanza bidhaa nzuri, pili ushindani. Bidhaa ya Nandy na Wasafi ni muziki, na kwa hakika pande mbili hizi zinafanya muziki mzuri. Kwa hiyo kinachokosekana hapa ni ushindani ambao mpaka sasa umebaki kama tetesi kwa sababu hakuna ambaye amekiri kuna ushindani.