Kanye West na Tidal ya JAY-Z hawapo pamoja tena. Kwa mujibu wa TMZ,
Yeezy amejiondoa kwenye kampuni hiyo kutokana na mgogoro wa kifedha na
Tidal imepanga kumshtaki. Vyanzo vimeuambia mtandao huo kuwa Kanye
hakuwa na furaha na kampuni hiyo kwa muda mrefu sasa. Kanye amekuwa
akilalamika kuhusu kulipwa kiasi cha dola milioni 3 anazoidai Tidal.
Vimesema kuwa mwezi mmoja uliopita, mwanasheria wake alituma barua
kwa Tidal akisema kuwa kampuni hiyo imekiuka makubaliano na kuusitisha
mkataba. Baada ya wiki mbili, wanasheria wa pande zote mbili walijaribu
kukaa chini kuzungumza tofauti hizo lakini juhudi ziligonga mwamba.
TMZ imesema baada ya wiki mbili, mwanasheria wa Kanye West
aliwatandika barua nyingine kusisitiza kuwa mkataba huo umeisha. Hata
hivyo uamuzi wa Kanye ulitangulia kuachiwa kwa album mpya ya Jay Z, 4:44
ambayo kwenye wimbo mmoja amemchana swahiba wake huyo wa zamani.
Bifu ya Kanye na Tidal ni kutokana na kushindwa kutumizwa kwa ahadi
kuwa baada ya album yake, The Life of Pablo kuvutia takriban watumiaji
wapya milioni moja kwenye mtandao huo na kwamba alipaswa kulipwa bonus
ambayo hadi leo hajapewa. Pia mume huyo wa Kim Kardashian anasema Tidal
imegoma kumrudishia gharama zake za kufanya video.
Hata hivyo Tidal imesema Yeezy alishindwa kuwasilisha video
zilizohitajika kwenye mkataba huku yeye akidai asingeweza kufanya hivyo
bila kupewa bajeti yake. Kampuni hiyo imempiga mkwara Kanye kuwa bado
ina mkataba naye na kama akisaini na huduma nyingine ya kusikiliza
muziki, watakutana mahakamani.
Yeezy anasema Tidal wakimshtaki, naye anawashtaki vile vile. Hatua
hiyo inazidi kutengeneza uadui mkubwa kati ya Kanye na JAY-Z ambao
waliwahi kutoa album ya pamoja, Watch The Throne.
No comments:
Post a Comment