Hatma ya kibarua cha nyota wa Barcelona, Neymar wiki hii kimezidi kuwa mashakani baada ya timu ya Paris Saint Germain kupanda dau wakimtaka kinara huyo na huku taarifa nyingine zikieleza kuwa kwake yeye binafsi anatafakari jinsi ya kuondoka wakati wa usajili wa majira haya ya joto.
Kwa sasa matajiri hao wa Jiji la Paris wametangaza kuwa wana ubavu wa kuvunja mkataba kwa kutoa kitita cha Euro milioni 222 ili kuhakikisha wanapata huduma ya nyota huyo kuanzia majira haya ya kiangazi.
Hata hivyo, kama dili hilo likifanikiwa halitawashangaza wengi kutokana na kwamba atakuwa si nyota wa kwanza kuondoka kwenye klabu hiyo ili kusaka maisha mapya.
Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya wachezaji mahiri ambao waliamua kuwatema vinara hao wa Catalan.
Ukianza na mwaka jana aliyeondoka alikuwa ni mlinda mlango, Claudio Bravo.
Staa huyo raia wa Chile aliondoka mwishoni mwa usajili wa majira ya joto yaliyopita na kwenda kujiunga na Manchester City ambao waliiahidi Blaugrana kitita cha pauni milioni 18.
Kuondoka kwa nyota huyo kunadaiwa ni kutokana na kutishwa na ujio wa staa mwingine, Marc-Andre ter Stegen.
Kabla ya kuondoka, Bravo ndiye aliyekuwa mlinda mlango namba moja wa Barcelona katika kipindi cha kati ya 2015 na 2016 ambapo waliweza kutwaa ubingwa wa michuano ya La Liga.
Pia msimu uliopita, Bravo si mchezaji pekee ambaye aliamua kuondoka akiwa mchezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza tangu alipowasili mwaka 2009.
Baada ya staa huyo kuondoka, mwingine aliyefuatia alikuwa ni Dani Alves, aliyekwenda kujiunga na Juventus akiwa ameshabeba mataji kadhaa ya ligi ya nyumbani na akaifikisha timu hiyo hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini akiwa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake akaenda kujiunga na PSG.
Staa mwingine aliyeamua kuitosa Barca alikuwa pia ni Cesc Fabregas ambaye aliondoka mwaka 2014.
Kuondoka kwa nyota huyo kulionekana kutoufurahisha uongozi wa klabu hiyo ya Catalan ambako staa huyo alianzia kibarua chake na hivyo wakaamua kumrejesha tena msimu wa 2011.
Pamoja na kurejeshwa nyota huyo alijikuta akishindwa kupata namba baada ya kushindwa kucheza na viungo wenzake, Xavi na Andres Iniesta.
Hata hivyo, nyota huyo alikuja kushindwa zaidi wakati timu hiyo ilipokuwa chini ya kocha Gerardo Martino ambaye alikuwa akimtumia mara kwa mara akicheza kama namba tisa ambayo haimudu na mwisho wake akaamua kuondoka kwa ada ya Euro milioni 33 na kwenda kujiunga na Chelsea.
Pia staa mwingine aliyeondoka alikuwa ni mlinda mlango, Victor Valdes, aliyeiaga klabu hiyo alikokulia Juni 2014, baada ya kutangaza kuwa hataweza kuongeza mkataba.
Wakati Valdes akiondoka alieleza kuwa anataka kwenda kujaribu bahati yake nje ya nchi lakini mambo hayakwenda kama alivyotarajia kutokana na kukumbana na majeraha ya goti wakati wa mchezo dhidi ya Celta Vigo na kumfanya ashindwe kujiunga na Monaco na tangu kipindi hicho soka lake likatetereka.
Pia Samuel Eto’o ni nyota mwingine ambaye alikuwa straika tegemeo katika kikosi hicho cha Blaugrana.
Nyota huyo aliitema klabu hiyo mwaka 2009 baada ya mwaka 2008 kuwa chini ya Pep Guardiola na ilishuhudiwa nyota wengine kama Ronaldinho na Deco wakiondoka.
Hata hivyo, baada ya kuondoka na kwenda kujiunga na Inter Milan akiwa sehemu ya mkataba, uongozi ulimleta Zlatan Ibrahimovic, nyota huyo aliweza kung’ara na kuwawezesha vinara hao wa nchini Italia kutwaa ubingwa wa michuano ya Ligi ya Mabingwa 2010.
Mastaa Deco na Ronaldinho waliondoka kwenye klabu hiyo mwaka 2008 wakiwa wameshatamba wakati klabu hiyo ya Camp Nou ilipotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa wakiwa chini ya kocha wao, Frank Rijkaard.
Wawili hao walikuwa tayari wameitumikia klabu hiyo kwa miaka mingi na walipoondoka Barcelona ambapo Ronaldinho alikwenda kujiunga na AC Milan na Deco akajiunga na Chelsea, Barcelona ilibaki na pengo ambalo liliichukua muda mrefu kuliziba.
Usajili wa Luis Figo wa ada ya pauni milioni 10 ulikuwa ni wenye utata katika historia ya soka.
Utata huo ulitokana na kwamba aliuzwa kwa pauni milioni 10 ili akajiunge na Florentino Perez katika kikosi cha Real Madrid.
Tangu kipindi hicho nyota huyo alikuwa akiandamwa na mashabiki wa Barcelona.
Baada ya nyota huyo kuondoka Barca iliamua kuwakuza Marc Overmars, Emmanuel Petit na Alfonso, lakini hakuna hata mmoja ambaye aliweza kupata mafanikio akiwa na klabu hiyo ya Camp Nou.
No comments:
Post a Comment