Na: Omary Ramsey
“Huwezi kuona msitu ukiwa msituni” Hakika ni upofu wa mashabiki wengi
ambao wamekuwa wakiamini kila neno kutoka kwa msanii wao Diamond
Platnumz.
Mashabiki wengi hawajui namna ya kuchanganua hoja, ila hoja zao
nyingi hutawaliwa na lugha kali isiyo na maana wala faida yoyote mbele
ya maisha yao, lakini siamini kama msanii husika anafurahishwa na
mashabiki wa aina hii.
Moja ya kauli ambayo Diamond Platnumz aliisema wiki kadhaa nyuma ni
“Sitegemei Radio na Runinga katika kufanya promosheni ya kazi zangu za
muziki.
Kauli hii ilizua maneno mengi hasa kwa watangazaji na madj wa Radio
na Runinga. Wapo ambao waliamua kutoa mitazamo yao kwenye vipindi vyao,
ila pia wapo ambao walitoa mitazamo nje ya vipindi yani katika vijiwe
vingi katika makutano tofauti.
Ni wazi huwezi kupinga ukubwa wa Diamond Platnumz katika bara la
Afrika na nje pia. Hivyo ana kila sababu ya kusema kila neno ambalo yeye
ataona linafaa kwa wakati huo. Lakini je anawaza juu ya wasanii wake?
Ni ukweli usiopingika kuwa wasanii wake ambao wapo chini ya Label
yake ya Wasafi bado sio wasanii wakubwa kama vile mashabiki
wanavyowajaza sifa wasizokuwa nao. Hawana ushawishi kama wa Diamond
Platnumz, ukweli ambao mashabiki wengi huupinga.
“Bora kujikwaa kidole kuliko ulimi” Huenda ni kweli sasa Diamond
hategemei Radio na Runinga katika kusukuma muziki wake, ila je vipi
kuhusu wasanii wake? Je!nao hawategemei Radio na Runinga kama Diamond?
Na aliamua kusema ili iweje?
“Fahari mama wa ujinga” Tangu kutoka kwa kauli yake Diamond Platnumz
tuliona hoja za wadau wengi katika mitandao ya kijamii hususani
Twitter.Wapo waliosifu kauli hiyo na wapo walioponda kauli hiyo. Na
daima hupaswi kupinga mtazamo wa mtu.
Kauli hii imeweza kumtafuna vyema msanii wake Harmonize huku wengine
wakisubiri kuona kwa wasanii wengine kutoka WcB vile itakuwa mara baada
ya kutoa nyimbo.
Ni siku chache tangu kutoka kwa wimbo wa Nambie wa Harmonize. Ila
katika kipindi kichache pia Harmonize hasikiki na wimbo wake licha ya
kuweza kumtumia mpenzi wake katika video yake, lakini pia mwanzoni
kutengeneza kiki ya kuachana ilhali tu wapate kuzungumziwa ila imekuwa
ndivyo sivyo……..
“Huwezi kwenda kwa jirani pasi kutokea kwako”
Itaendelea..
No comments:
Post a Comment