Aliyekua mshambuliaji wa klabu ya Arsenal Thierry Henry ameshindwa
kusema lolote kuhusu mpango wa kufikiriwa kuwa mrithi wa meneja wa sasa
wa klabu hiyo Arsene Wenger, ambaye huenda akaondoka mwishoni mwa msimu
huu.
Wenger bado hajazungumza kuhusu mustakabali wake klabuni hapo, lakini
mkataba wake utafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, huku kukiwa ma
tetesi huenda akasaini mkataba mwingine wa mwaka mmoja hadi miwili.
Gazeti la Daily Telegraph limeripoti kuwa, Henry amekua mmoja wa watu
wanaopewa kipaumbele cha kukabidhiwa benchi la ufundi la Arsenal, na
msimamo huo unashikiliwa na mtoto wa tajiri Stan Kroenke anaemiliki
asilimia kubwa ya hisa za klabu ya Arsenal aitwae Josh.
Kwa sasa Henry anafanya kazi kama kocha msaidizi wa timu ya taifa ya
Ubelgiji sambamba na Roberto Martinez, ambaye alikabidhiwa jukumu la
kuwa mkuu wa benchi la ufundi la timu hiyo mwaka jana.
Henry aliwahi kuwa kocha wa kikosi cha vijana cha Arsenal, kabla ya
kukorofishana na Arsene Wenger kufuatia kazi ya uchambuzi wa soka
aliyokua akiifanya kwenye kituo cha televisheni cha Sky Sports, ambapo
mara kadhaa alikuwa akieleza wazi wazi mapungufu ya klabu hiyo upande wa
kikosi cha wakubwa.
Mshambuliaji huyo anaendelea kukumbukwa na mashabiki wa Arsenal kwa
uwezo wake wa kucheza soka nafasi ya ushambuliaji, na wakati wa utawala
wake alifanikiwa kufunga mabao 228.
No comments:
Post a Comment