Thursday 12 October 2017

Ujumbe muhimu kwa binti mwenye nia ya dhati ya kuolewa



Akina dada wengi wanapenda sana kuolewa; lakini ni wachache sana wanajua namna ya kukaa mkao wa kuolewa, na pia namna ya kuchambua kati ya mwanaume muoaji na mwanaume muonjaji. 

Maua yana tabia ya kujifunga, lakini yanajua pia muda sahihi wa kuchanua na kutoa harufu inayowavutia nyuki; lakini cha ajabu akina dada wa digitali hatujui haya, tunazidiwa akili na maua. 

Hii ni hatari sana. Ninapozungumzia muda wa ua kuchanua na kutoa harufu inayovutia nyuki; namaanisha uwezo wa kutambua majira sahihi ya dada kuolewa na kuhama toka kwenye kundi la "Maua yaliyojifunga" yaani usichana kuingia kwenye maua yanayoingia kwenye "Uchavushaji" yaani kuwa mke, mama nakadhalika. 

Nyuki hawawezi kuruka kuja kwenye ua lililojifunga (mdada aliyekaa mkao wa kutoonesha dalili za kuwa mke), bali nyuki huwa wanaruka kuelekea kwenye maua yaliyochanua na yenye harufu ya kuvutia. 

Kama dada, kama unaona muda wako wa kuolewa uliokusudia umekaribia, anza "Kuchanua" anza kujenga tabia za mke na si sista duu anayetafuta mme. Nyuki wote wanajua maua yaliyochanua na yenye harufu nzuri; vivyo hivyo kwa wanaume waoaji, nao wanajua binti gani anafaa kuwa mke. 

Tabia na mfumo wa kuwa mke haujengwi ndani ya ndoa; unajengwa ukiwa bado peke yako, unaanza kupunguza tabia zisizohitajika kwenye ndoa ambazo mabinti wa kawaida huwa wanakuwa nazo. 

Unaanza kujenga tabia ya kuwa mama mwenye nyumba, jifunze kuwa katika namna ya mke apaswavyo kuwa. Ukikaa kwenye uhalisia wa mke atakiwavyo kuwa; nyuki wataona na watakuja, halafu wewe ndiwe utakayekuwa na kazi ya kuchagua yupi kati yao ni muoaji na yupi kati yao ni muonjaji. 

Kila mwanadada aliyekusudia kuolewa anaweza kuolewa, lakini ni lazima uwe na ufahamu wa kutosha kuhusu mke apaswavyokuwa kabla hauja-attract attention ya waoaji. Mungu awasaidie akina dada wenye nia ya dhati ya kuolewa na kuwa na miji yenu.

No comments:

Post a Comment