Tuesday 5 September 2017

Makala: Kwani Kiba, Diamond ni wapinzani?




Tangu mwimbaji Ally Kiba arejee kwenye Bongo Fleva na kibao chake cha Mwana Dar es Salaam mwaka 2014, baada ya kupumzika kwa takribani miaka miwili, mashabiki wa muziki nchini wamekuwa wakivuta juu ya nani zaidi kati ya msanii huyo na mwenzake Nasib Abdul ‘Diamond’.

Upinzani huo unaosababishwa na mashabiki wa Bongo Fleva umekuwa kikwazo kikubwa kwa wasanii wengine wa muziki huo, hasa pale wasanii hao wanapotoa nyimbo zao.

Hiyo inatokana na mashabiki wengi na hata vyombo vya habari kuwaangalia wasanii hao wawili na kuwapotezea wengine, jambo linalowaua kisanii kwa kukosa sapoti na promo.

Pamoja na hayo yote ni kweli kwamba wasanii hao wanashindana? Hilo ni swali ambalo jibu lake ni rahisi sana kwa kuwa wasanii hao hawana vitu ambavyo vinawafanya washindane hata kama kutakuwa kuna mmoja anayejaribu kuulazimisha ushindani.

Hivi ni kweli kama kungekuwa na ushindani kati ya wasanii hao wawili, mmoja angekuwa ametoa jumla ya nyimbo nne tangu aliporudi kwenye muziki mwaka 2014?

Wakati mmoja ametoa nyimbo nne, ambazo ni Mwana Dar es Salaam, Chekecha, Lupela na hii ya sasa Seduce Me, kuanzia kipindi hicho cha kutoka mwaka 2014 hadi mwaka huu, mwingine nyimbo 14.

Nyimbo hizo ni Marry You, Kidogo, Salome, Number One na Eneka, Bum Bum, Nana, Fire, I Miss You, Moyo Wangu, Acha Nikae Kimya, Nataka Kulewa, I Will Marry You ukiachana na zile alizoshirikishwa kama Love Boat, Wangu na My Heart.

Nyimbo hizo 14 ni zile ambazo amefanya mwenyewe, huku kwa kipindi hicho hicho mwingine ameshirikishwa kwenye nyimbo takribani tatu, ambazo ni Jike Shupa na Nuh Mziwanda, Mboga Saba ya Mr Blue na Unconditionally Bae ya wasanii wa Kenya, Sauti Sol.

Hilo ni moja ya jambo linaloonyesha kwamba wasanii hao hawana upinzani, kwani kama wangekuwa wanao basi Kiba asingekuwa anaendelea na mambo yake wakati mwenzake anadondosha idadi kubwa ya nyimbo kama hizo.

Hapo hakuna upinzani, kama ungekuwapo upinzani wowote, basi lazima mmoja angeshapotea kwenye tasnia hiyo ya muziki kutokana na mwenzake anavyotoa nyimbo nyingi yeye akitoa wimbo mmoja kwa mwaka.

Lakini ukitaka kujua wawili hao hawana upinzani wowote, angalia kila mmoja anapotoa wimbo upande wa pili unahangaika kumfunika na mara zote wamekuwa wakishindwa.

Ndio inasumbuka, kwanini huyu mwingine hajawahi hata mara moja kutoa wimbo baada ya mwenzake kutoa, lakini kila mwaka msanii mmoja amekuwa akimfanyia mwenzie hivyo.

Mfano ni wimbo wa Seduce Me, saa 12 baada ya kutoka upande wa pili ukatoa wimbo ingawa huu uliwashirikisha wanafamilia nzima ya lebo’ yao ni wazi kwamba walitaka kumfunika mwenzao, lakini mambo hayakwenda kama walivyotarajia.

Kukwama kufunika wimbo wa Seduce Me kwa kutoa kibao cha Zilipendwa imeonyesha wazi kwamba, kuna msanii anashinda na mtu asiyeshindana naye ni kama anapigana na kivuli cha mwenzake.

Wasanii hawa wako tofauti sana, ukianzia uvaaji wao na mwonekano hata uwezo wa kuimba, kuna mmoja ana damu ya nguo, hahitaji kuvaa nguo nyingi au kuingia gharama ya nguo nzuri ili apendeze bali aina yoyote ya nguo anayoivaa inampendeza tofauti na mwingine ambaye ilibidi atafute mtu wa kumfundisha namba ya kuvaa angalau awe na mwonekano mzuri, jambo ambalo lilimsaidia kwa kiasi fulani.

Pia wanatofautiana kwenye uchaguzi wa aina ya nguo pamoja na kutambua mazingira ya kuvaa nguo zao, hata maisha yao yako tofauti, kuna mmoja anataka kila anachokifanya kijulikane kwenye vyombo vya habari ili kimsaidie kwenye muziki wake, mwingine maisha yake ya kimuziki na yale binafsi ni vitu viwili tofauti.

Maisha binafsi ya msanii mmoja yanabaki kuwa siri hata kama akiwa na mpenzi yanakuwa ni maisha yake binafsi na hayahusiani kabisa na muziki wake.

Mwisho kwenye uwezo wa kuimba hasa kwa kutumia vyombo ‘live’, kuna mmoja anaweza kufanya kwa ufasaha, huku mwenzake ameshindwa kuonyesha hilo kwenye matamasha kadhaa na kila mara alipojaribu kuimba ameimba nje ya ufunguo (key) ama nje ya mdundo wa muziki (beat). Wasanii hawa wawili si wapinzani, kama upo basi kuna upande mmoja unalazimisha.

No comments:

Post a Comment