Saturday 22 July 2017

Makala: Kumbe Mourinho hayuko kihivyo




Kwa muda mrefu kocha Jose Mourinho amekuwa akitajwa kuwa huwa hapendi kuwatumia wachezaji chipukizi.
Dhana hiyo inatokana na kwamba katika timu ambazo amepitia mara nyingi amekuwa akisajili wachezaji wenye majina, huku akiwatosa ambao wapo kwenye vikosi vya timu za vijana.
Hata hivyo, kwa sasa dhana hiyo inaonekana kuwa haipo tena, baada ya utafiti kuonesha kuwa msimu uliopita ndiye aliyetumia chipukizi wengi kuliko timu yoyote ya Ligi Kuu England, licha ya kuwa hawakupata muda mwingi wa kucheza. 
Katika utafiti huo uliofanywa na jarida la PA, msimu uliopita Mourinho aliwatumia wachezaji 10 kutoka katika  timu ya vijana. 
Makinda hao ni Joel Pereira, Demetri Mitchell na Josh Harrop ambao waliweza kucheza sehemu ya mechi moja moja na huku kinda Scott McTominay akicheza dakika 96 msimu mzima na  Timothy Fosu-Mensah akacheza 94.
Katika kikosi chake hicho, Angel Gomes, alikuwa mchezaji wa kwanza kuzaliwa karne ya 21, lakini aliweza kucheza dakika mbili tu. 
Katika orodha hiyo ya wachezaji waliokulia kwenye klabu hiyo alikuwa ni  Paul Pogba ambaye aliruhusiwa kuondoka baada ya kuchomoza kwenye kikosi cha kwanza na kisha akasajiliwa tena kurejea majira ya joto yaliyopita kwa ada ya pauni milioni 89. 
Katika utafiti huo pia Arsenal ndiyo iliyoongoza kwa kuwapa muda mwingi wa kucheza wachezaji ambao iliwakuza. 
Mastaa hao ni Hector Bellerin, Francis Coquelin, Alex Iwobi, Kieran Gibbs, Emiliano Martinez na Ainsley Maitland-Niles ambao kwa pamoja walicheza kwa muda wa dakika 6,628 ambazo ni sawa na asilimia 19.4  ya muda ambao  Gunners iliutumia uwanjani. 
Kwa upande wao Burnley na Swansea City zenyewe hazikuweza kuyatumia mazao yake zilizoyalea wakati timu za
Bournemouth, Liverpool na Stoke City zenyewe ziliwapa asilimia moja ya kucheza.
Manchester City wao walimtumia mchezaji mmoja ambaye ni  Kelechi Iheanacho, waliyempa muda wa dakika  526 sawa na asilimia 1.4  na huku ikiwapa nafasi finyu wachezaji waliokulia Uingereza kwa asilimia 14  na wa Ulaya nzima asilimia 59. 
Katika msimu huo Man City pia iliwatumia wachezaji wanne ambao walikulia kwenye shule za timu za vijana za Uingereza ambao ni Raheem Sterling (Liverpool), John Stones (Barnley) na  Fabian Delph (Leeds).
Katika orodha hiyo timu kubwa zilizoshika nafasi za mwanzo ambazo ni  Chelsea, Tottenham, City, Liverpool, Arsenal na United zilishika nafasi ya mwisho kwa kuwapa muda wa dakika nane makinda wake waliokulia katika shule za timu za vijana za Uingereza.
Bournemouth wao ndio wanaoshika nafasi ya juu kwa kuwatumia wachezaji waliokulia Uingereza ambapo ina asilimia 90.3 katika muda ambao walicheza kila mechi.
Burnley wao wanashika nafasi ya pili wakiwa na asilimia 85 na vile vile ndiyo timu ambayo iliongoza kwa kuwatumia wachezaji wengi waliokulia katika klabu za soka Ulaya.

No comments:

Post a Comment